Monday, 22 July 2013

JK kuwaaga wanajeshi waliouawa.

RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuongoza mamia ya waombolezaji kuiaga miili ya wanajeshi saba wa Tanzania waliouawa nchini Sudan wiki iliyopita.

Wanajeshi hao walikuwa miongoni mwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan. Walivamiwa na kushambuliwa kwa risasi na waasi.

Akizungumzajana jijini Dar es Salaam kwa njia ya simu, Kaimu Msemaji wa jeshi hilo, Meja Joseph Masanja, alisema kuwa maandalizi yamekamilika na leo majira ya saa 2:30 asubuhi miili hiyo itaagwa waombolezaji wakiongozwa na Rais Kikwete pamoja na viongozi wengine wa kitaifa.

“Maandalizi yote yamekamilika. Kutakuwa na shughuli ya kuaga miili na baadaye tunasafirisha kwenda makwao kulingana na matakwa ya familia zao,” alisema.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliwaongoza wananchi kuipokea miili hiyo iliyowasili juzi kwenye viwanja vya jeshi vya Air Wing, jijini Dar es Salaam.

Wanajeshi waliouawa ni Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Juma, Koplo Mohamed Chikilizo, Rodney Ndunguru, Peter Werema na Fortunatus Msofe.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za jeshi, hii ni mara ya pili kwa wanajeshi wa Tanzania kuuawa nchini humo. Awali ilikuwa Agosti mwaka jana ambapo wanajeshi watatu waliuawa.
Tanzania ina askari 850 kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika Jimbo la Darfur, ambao ni sehemu ya askari 1,081 wa kulinda amani katika jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment