AGNES JERALD
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzoa, alisema haijafahamika wanawake hao wanatoka mikoa gani.
Kamanda Nzoa aliwataja wanawake hao kuwa ni Agnes Jerald ambaye alisema hajapiga hesabu ya umri wao, ila alizaliwa mwaka 1988 kwa maana hiyo ana umri wa miaka 25 na Melisa Edward ambaye alisema amezaliwa mwaka 1989 kwa maana hiyo atakuwa na umri wa miaka 24. Wawili hao bado wanaendelea kuhojiwa na polisi wa Afrika Kusini.
Alisema Jeshi la Polisi Nchini kwa upande wake linaendelea kufanya uchunguzi kubaini kama dawa hizo walitoka nazo wapi na pia linawasaka watu ambao watakuwa ndiyo wamiliki wa dawa hizo.
Jumapili iliyopita NIPASHE ilipata taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani hiyo nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa kutoka Tanzania.
Taarifa hizo zilionyesha kuwa wanawake wawili walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oriver Tambo uliopo eneo la Kempton Park siku ya Ijumaa wiki iliyopita wakitokea Tanzania.
Wanawake hao walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini wakiwa na masanduku sita ambayo yalipokaguliwa yalikutwa na takribani kilo 150 za dawa hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’ zikiwa na thamani ya bei ya mtaani ya Randi milioni 42 sawa na Sh. bilioni 6.8.
Baada ya kukamatwa na dawa hizo wanawake hao walikabidhiwa polisi.
Tukio hilo linatoka takribani wiki moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Juni 28, mwaka huu kutangaza kuwa tatizo la dawa za kulenya hivi sasa ni janga la kitaifa nchini.
Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
Pia alisema katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, na hivyo kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Pinda alisema mwaka huu pekee kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya katika eneo la kimataifa la Bahari ya Hindi karibu na Tanzania.
Alisema hivi sasa mikate, maandazi na askrimu zinazouzwa kwenye shule za msingi, zinawekwa dawa za kulevya.
Alisema vitendo hivyo vinafanya vijana wengi wa shule za msingi na hata sekondari kuwa na tabia za ajabu, ikiwamo kuingia darasani wakiwa na kiatu kimoja mguuni, mkufu wenye nyembe na kidani chenye nyembe kifuani.
No comments:
Post a Comment