Saturday, 6 July 2013

AUNT, WOLPER: TUTAWAUA WABUNGE WENU SIKU YA KESHO TAIFA.

Aunt Ezekiel.
Na Mwandishi Wetu
NI mshikemshike kwa ajili ya Tamasha la Matumaini, Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo mastaa wa filamu za Kibongo wanaoshiriki ndondi na wabunge, Aunt Ezekiel na Jacqueline Wolper wametamba kuwamaliza waheshimiwa hao.
 
                                                                   Jacqueline Wolper.
AUNT VS ESTER BULAYA
Aunt ambaye atazichapa na Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mara (CCM), Ester Bulaya ameapa kuwa lazima siku hiyo ‘amuue’ mheshimiwa huyo kwa madai kuwa kwa sasa yupo fiti baada ya kurejea kutoka kambini, Dubai.
Alisema kuwa amepata mazoezi ya nguvu ya kurusha na kupangua ngumi kutoka kwa mwalimu wake, Abdul Al-Mohd ambaye amempa mbinu zote za kummaliza mbunge huyo katika raundi za mwanzo.
 
                                                                          Ester Bulaya.
“Nipo fiti sana, najua mheshimiwa Ester ni mtu wa Mara kwa wakorofi na ana hasira lakini hilo halinipi shida, cha msingi mashabiki wangu waje kushuhudia nikimmaliza mtu,” alisema Aunt na kuongeza:
“Ester ni mwanasiasa mzuri na ana mazoea na majukwaa ya siasa lakini mimi nataka niwathibitishie watu kuwa naweza kumiliki ulingo vilivyo kama ninavyokuwa stejini.
 
                                                                    Halima Mdee.
“Kazi ni moja tu keshokutwa (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, natoa tahadhari kuwa ‘nitamuua’ mbunge wenu. Nawaahidi mashabiki wangu na watu wote ushindi ‘so’ wote tukusanyike tupate burudani na kuchangia elimu yetu.”


WOLPER VS HALIMA MDEE
Kwa upande wake, Wolper ambaye atazichapa na Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ametamba kuwa yupo fiti katika kiwango chake cha juu kabisa cha mazoezi ya ndondi hivyo anachosubiri ni kukutana na mpinzani wake ammalize.
Wolper aliyekuwa kambini nchini Afrika Kusini akipata mbinu kutoka kwa mwalimu wake nchini humo, alisema kwa sasa yupo fiti chini ya uangalizi wa mwalimu wake wa muda ambaye ni mwigizaji Jacob Steven ‘JB’.
Zitto Kabwe.
“Halima yeye ni mwanasiasa, najua ni mtu wa maneno mengi kwenye majukwaa ya siasa. Mimi kazi yangu ni kuigiza na kupiga ngumi hadi mtaani sasa hivi wananiita bondia,” alisema Wolper na kuongeza:
“Mimi ni bondia kweli. Nadhani mliniona mwaka jana nilipozichapa na Wema Sepetu. Naomba wapigakura wa Kawe wawe tayari kwa lolote litakalotokea kwa sababu lazima nimzimishe mbunge wao. Tunakwenda pale kwa kazi moja tu, ‘kuwaua’ wabunge wenu.”
Hata hivyo, Wolper aliwataka mashabiki wake na watu wote kukusanyika Uwanja wa Taifa kushuhudia ngumi za kufa mtu na burudani nyingine kibao.
Vincent Kigosi ‘Ray’.
MASTAA WENGINE
Mastaa wengine watakaonyukana ni mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’ na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ambao kila mmoja anaendelea na mazoezi mazito huku JB akitaka kuzichapa na Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan ili ampige kwa KO.
Katika ndonga za ‘maprofesheno’, Mkenya Patrick Amote atanyukana na Mtanzania Thomas Mashali huku Shadrack Muchanje wa Kenya akitoana nundu na Francis Miyeyusho wa Bongo.

No comments:

Post a Comment