MAKOCHA wa kigeni, ambao wamewahi kuifundisha Simba na Yanga
wamechambua uamuzi uliofanywa na klabu ya Msimbazi kwa kumuacha kipa wao
namba moja, Juma Kaseja.
James Siang’a
Kocha wa zamani wa Simba, James Siang’a amesema
Simba imefanya kosa kubwa kumuacha Juma Kaseja katika usajili wake na
kwamba watajutia mbele ya safari.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka kwao Bungoma,
Kenya jana Jumatatu, Siang’a alisema: “Kaseja ni Simba damu, ana uwezo
mkubwa na pia ana uzoefu mkubwa.”
Siang’a alisema ipo siku Simba watarudi
kumbembeleza Kaseja, lakini kipa huyo atawapa masharti magumu na
watashindwa kumchukua hivyo ni vyema wabadilishe uamuzi sasa na kuwa
naye kwa msimu mwingine zaidi.
“Sidhani kama Simba wamemuacha kwa sababu ya uwezo. Nimekaa na Kaseja namjua vizuri, huenda alitaka fedha nyingi, lakini lilikuwa jambo jepesi tu la kumalizana naye,” alisema.
Siang’a, ambaye amewahi kuwa kipa wa Harambee
Stars, aliishauri Simba kumsomesha Kaseja ili awe kocha wa makipa wa
timu hiyo ya Msimbazi.
“Tena siku hizi kuna mafunzo ya makocha wa makipa.
Simba kama wamemchoka wampe nafasi hiyo ili aje kuwa kocha wa makipa
siku za baadaye,” alishauri.
Kosta Papic
Kocha wa zamani wa Yanga, Kosta Papic alisema
Kaseja asiwe na wasiwasi kwani kwa uwezo wake, lazima atapata timu kubwa
ya kuichezea.
Papic, ambaye alizungumza na Mwanaspoti akiwa Afrika Kusini alisema katika hali ya kawaida Si
“Ninachohisi, Kaseja atakuwa ametaka fedha nyingi ndio maana
Simba wameamua kuachana naye, sidhani kama wangemuacha bila sababu ya
msingi,” alisema Papic.
“Unapokuwa na kiongozi katika timu unajivunia,
unapoitaja Simba unamtaja Kaseja, sijui itakuwaje kwa Simba kwa sababu
wanampoteza kiongozi wao uwanjani, inaweza kuwasumbua msimu ujao.
“Lakini huenda Simba wanataka damu changa,
wanataka mageuzi, kwa hiyo kwa upande mwingine pia huwezi kulaumu, kwa
sababu wao ndio wanajua sababu. Hata hivyo Kaseja atapata timu nzuri kwa
sababu ana kiwango kizuri,” alisema Papic, ambaye sasa ni kocha wa
Black Leopard ya Afrika Kusini, iliyoshuka daraja na ana kazi ya
kuipandisha Ligi Kuu Afrika Kusini msimu ujao.
Milovan Cirkovic
Kocha ambaye mashabiki wa Simba wanalaani
kutimuliwa kwake, Milovan Cirkovic amepinga uamuzi wa kamati ya usajili
kumtema kipa namba moja wa Tanzania, Kaseja.
Milovan alisema: “Nafikiri wamefanya kosa
kumuacha. Naamini Kaseja bado ni kipa mzuri na anajua majukumu yake
ipasavyo. Ndiyo maana mpaka sasa yuko katika timu ya Taifa Stars.”
“Anaweza akapata timu kubwa nje ya Tanzania. Ni
kipa aliyejenga vizuri jina lake kisoka, ni jambo la kushtua na
kukatisha tamaa ingawa anatakiwa kulichukulia kama changamoto katika
maisha yake ya soka.”
Sredejovic Milutin ‘Micho’
Kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Sredejovic
Milutin ‘Micho’ alisema ana uhusiano mzuri sana na Simba na akasema
anaheshimu kila wanachokifanya.
“Kwangu mimi nashukuru kwamba kipa wangu wa timu
ya taifa ya Uganda, Abeil Dhaira atapata nafasi ya kucheza na kuonyesha
kiwango chake Simba, hata hivyo ningependa aonyeshe kiwango chake kwa
kupambana na Kaseja na si kwa sababu Kaseja ameondoka,” alisema kwa
kifupi kocha huyo wa zamani wa Yanga huku akisisitiza kuwa Simba
inapaswa pia kuangalia masilahi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
ViaMwanasport.
ViaMwanasport.
No comments:
Post a Comment