Saturday, 6 July 2013

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwachezesha wabunge wa Simba, Yanga kesho

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Matumaini ambalo litafanyika kesho Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mbali ya kuwa mgeni rasmi, Rais Kikwete ambaye ni mdau mkubwa wa michezo ya soka na kikapu, anatarajiwa kuwa mwamuzi wa mchezo wa soka ambao utawakutanisha wabunge wa Simba watakaopepetana na wenzao wa Yanga, ikiwa ni sehemu ya tamasha hilo.
Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho, Rais Kikwete amekubali kuwa mgeni rasmi ambapo atachezesha mechi hiyo na kutoa neno la matumaini mwa maelfu ya watu watakaojitokeza uwanjani hapo.

“Rais Kikwete amekubali ombi letu la kuwa mgeni rasmi, pia atashika kipenga na kuchezesha mechi ya wabunge kwa dakika kadhaa, ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa,” alisema.
Katika tamasha hilo kutakuwa na burudani na michezo mbalimbali na litaanza saa nne asubuhi na kufikia tamati saa sita usiku.
“Mchezo mwingine wa soka siku hiyo utakuwa kati ya Bongo Fleva dhidi ya Bongo Movie, burudani nyingine ni mapambano ya ndondi kati ya mwigizaji Aunt Ezekiel dhidi ya Mbunge Ester Bulaya, staa mwingine wa filamu Jacqueline Wolper atapigana na Mbunge Halima Mdee, Mbunge Zitto Kabwe atachapana na Vincent Kigosi ‘Ray’,” alisema Mrisho.
 Alisema mbali na mapambano hayo ya burudani, kutakuwa na mapambano ya ukweli kati ya Francis Miyeyusho dhidi ya Shadrack Muchanje, Thomas Mashali dhidi ya Patrick Amote.
 Mrisho aliongeza kuwa kutakuwa na burudani ya wanamuziki wengi, baadhi yao ni rapa wa Kenya, Jackson Makini ‘Prezzo’ na Naasib Abdul ‘Diamond’.

No comments:

Post a Comment