RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuongoza mamia ya
waombolezaji kuiaga miili ya wanajeshi saba wa Tanzania waliouawa nchini
Sudan wiki iliyopita.
Wanajeshi hao walikuwa miongoni mwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha
kulinda amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan. Walivamiwa na
kushambuliwa kwa risasi na waasi.
Akizungumzajana jijini Dar es Salaam kwa njia ya
simu, Kaimu Msemaji wa jeshi hilo, Meja Joseph Masanja, alisema kuwa
maandalizi yamekamilika na leo majira ya saa 2:30 asubuhi miili hiyo
itaagwa waombolezaji wakiongozwa na Rais Kikwete pamoja na viongozi
wengine wa kitaifa.
“Maandalizi yote yamekamilika. Kutakuwa na shughuli ya kuaga miili na
baadaye tunasafirisha kwenda makwao kulingana na matakwa ya familia
zao,” alisema.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliwaongoza wananchi
kuipokea miili hiyo iliyowasili juzi kwenye viwanja vya jeshi vya Air
Wing, jijini Dar es Salaam.
Wanajeshi waliouawa ni Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Oswald Chaula,
Koplo Mohamed Juma, Koplo Mohamed Chikilizo, Rodney Ndunguru, Peter
Werema na Fortunatus Msofe.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za jeshi, hii ni mara ya pili kwa wanajeshi
wa Tanzania kuuawa nchini humo. Awali ilikuwa Agosti mwaka jana ambapo
wanajeshi watatu waliuawa.
Tanzania ina askari 850 kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda
amani katika Jimbo la Darfur, ambao ni sehemu ya askari 1,081 wa
kulinda amani katika jimbo hilo.